Instagram

This is default featured slide 3 title

Go to Blogger edit html and find these sentences.Now replace these sentences with your own descriptions.This theme is Bloggerized by Lasantha Bandara - Premiumbloggertemplates.com.

This is default featured slide 4 title

Go to Blogger edit html and find these sentences.Now replace these sentences with your own descriptions.This theme is Bloggerized by Lasantha Bandara - Premiumbloggertemplates.com.

This is default featured slide 5 title

Go to Blogger edit html and find these sentences.Now replace these sentences with your own descriptions.This theme is Bloggerized by Lasantha Bandara - Premiumbloggertemplates.com.

Wednesday, August 21, 2013

Victor Wanyama amroga bosi Southampton


  Victor Wanyama.

Wanyama, Mkenya wa kwanza kucheza ligi hiyo, wikiendi iliyopita alicheza kwa dakika zote 90 katika mechi ya fungua dimba ya msimu mpya dhidi ya West Bromwich Albion ambapo timu yake ilishinda bao 1-0.

NI kama amerogwa. Kocha wa klabu ya Southampton ya Ligi Kuu England, Mauricio Pochettino, amekiri kuwa anatarajia makubwa kutoka kwa Mkenya, Victor Wanyama, ambaye wikiendi iliyopita alianza kuonyesha makali yake kwenye ligi hiyo maarufu katika anga la soka duniani.
Wanyama, Mkenya wa kwanza kucheza ligi hiyo, wikiendi iliyopita alicheza kwa dakika zote 90 katika mechi ya fungua dimba ya msimu mpya dhidi ya West Bromwich Albion ambapo timu yake ilishinda bao 1-0.
Baada ya kumpanga Mkenya huyo na kumfuatilia kwa makini uwanjani, kocha huyo ameiambia tovuti ya klabu hiyo akisema: “Wanyama ameonyesha kiwango kikubwa, ni mechi yake ya kwanza lakini ameonyesha na kwa kiasi gani mchango wake utahitajiwa msimu huu.
“Amekuwa na ushirikiano mzuri na wenzake na hiki ndicho kitu kilichotufanya tumsajili. Huu ni mwanzo naamini mambo yataongezeka kuwa mazuri.”
Kiungo huyo ambaye pia nahodha wa Harambee Stars, katika mechi hiyo alikuwa nguzo muhimu akikumbushia enzi zake alipokuwa Celtic ya Scotland.
Bao la ushindi la timu yake lilifungwa na Rickie Lambert katika dakika ya mwishoni.

Siri za mkataba wa Ngassa na Simba zafichuka rasmi


Mrisho Ngassa  

  WAKATI Mrisho Ngassa amepitishwa kuichezea Yanga msimu ujao wa Ligi Kuu Bara, imedhihirika kuwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) liliupokea mkataba wa Simba tangu Desemba 17, mwaka jana.
Habari kwa Vina imeuona mkataba wa Simba na Ngassa, ambao umegongwa muhuri wa TFF kuonyesha kuwa ulipokelewa katika shirikisho hilo tangu Desemba 17 mwaka jana.
Mkataba huo, unaonyesha kuwa Ngassa alisaini kuichezea Simba Agosti 2, mwaka jana na kwamba ulitakiwa uanze kutumika Mei 22 mwaka huu na kumalizika Mei 31 mwakani.
Katika moja ya makubaliano kwenye mkataba huo, Ngassa haruhusiwi kuichezea Yanga katika kipindi hicho au timu nyingine yoyote na mshahara wake ungekuwa Sh2 milioni kwa mwezi.
Hata hivyo katika kikao chake cha mwishoni mwa wiki, Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Soka (TFF), chini ya Alex Mgongolowa ilimuidhinisha Ngassa kuchezea Yanga, lakini ikamfungia mechi sita pamoja na kumtaka arejeshe Sh30 milioni ambazo alichukua Simba pamoja na asilimia hamsini ya fidia ambazo ni Sh15 milioni.
Kamati hiyo ilibaini kuwa Ngasa alisaini mkataba mwingine Simba (katika kipindi ambacho alikuwa na mkataba na Azam) na anatakiwa kurejesha fedha alizopokea Msimbazi Sh30 milioni pamoja na fidia ya asilimia 50 (Sh15 milioni) ya fedha hizo hivyo kufanya awe anadaiwa Sh 45 milioni.
Kamati hiyo pia imemfungia mechi sita za mashindano (kuanzia mechi ya Ngao ya Jamii Jumamosi iliyopita), na anatakiwa awe amelipa fedha hizo ndani ya kipindi hicho cha kukosa mechi hizo. Akishindwa, hataruhusiwa kucheza hadi atakapolipa fedha hizo.
Hiyo ina maana kuwa Ngassa amekosa mechi ya Ngao ya Jamii dhidi ya Azam na nyingine tano za Ligi Kuu Bara ambazo ni dhidi ya Ashanti, Coastal Union, Mbeya City, Prisons na Azam.
Kwa mara ya kwanza, Ngassa ataonekana katika Ligi Kuu Bara, Yanga itakapocheza dhidi ya Ruvu Shooting Septemba 28 katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

JK ataka vyuo vikuu nchini kudahili wanafunzi wengi


            Rais Jakaya Kikwete

Dar es Salaam. Rais Jakaya Kikwete amevitaka vyuo vikuu nchini kuweka nguvu zaidi, kuhakikisha vinadahili wanafunzi wa shahada za juu ili kupata wahadhiri.
Akizungumza baada ya kutoa hati idhini kwa Vyuo Vikuu na Vyuo Vikuu Vishiriki vinane, Rais Kikwete alisema kufanya hivyo vitakabiliana na tatizo la uhaba wa wahadhiri linalovikabili hivi sasa.
“Pale kwenye upungufu tusisite kutafuta wataalamu wengine kutoka nje ya nchi. Wakati wa miaka ya 1970 tulipokuwa tunasoma pale Chuo Kikuu (Mlimani), tulikuwa na wahadhiri wengi kutoka nje,” alisema Rais Kikwete.
Licha ya suala hilo, Rais Kikwete alisisitiza umuhimu wa vyuo hivyo kuwekeza kwenye utoaji elimu bora.
“Ikumbukwe idadi kubwa ya wanafunzi haitoshi, lazima tuzingatie ubora. Tunataka mwanafunzi anayepata shahada nchini ajulikane popote anapokwenda,” alisema Rais Kikwete na kuongeza:
“Isiwe shahada ya kibongobongo, akifika nje anaonekana kama ana stashahada.”
Pia, alisema kuna changamoto kubwa ya upatikanaji wa wanafunzi wa kutosha kujiunga na vyuo vikuu.
Alisema nafasi za vyuo vikuu kwa mwaka ni zaidi ya 78,000, lakini wanaopatikana ni 43,000, changamoto ambayo lazima wakabiliane nayo.
Alisema idadi ya wanafunzi wanaojiunga na vyuo vikuu nchini ni ndogo, ikilinganishwa na wanaojiunga na taasisi hizo kwa nchi nyingine.
Rais Kikwete aliiagiza Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kuhakikisha inatekeleza kwa ufanisi, mpango wa Matokeo Makubwa Sasa ( Big Result Now). Alivitaka vyuo hivyo kuhakikisha vinajitafutia njia nyingine za mapato, badala ya kusubiri karo.
Vyuo vilivyopata Hati Idhini ni Chuo Kikuu cha Tumaini Makumira (Tuma), Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino Tanzania (Saut) na Chuo Kikuu Kishiriki cha Ruaha (Ruco). Vingine ni Chuo Kikuu cha Mount Meru (MMU), Chuo Kikuu cha Arusha (UOA), Chuo Kikuu Kishiriki cha Tumaini Dar es Salaam (Tudarco), Taasisi ya Afrika ya Nelson Mandela ya Sayansi na Teknolojia, Arusha (NM-AIST) na Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (Must).

Mwakyembe awashukia wapelelezi dawa za kulevya!


Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe  


Dar es Salaam. Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe amewashukia waendesha mashitaka na wapelelezi kesi zinazohusiana na dawa za kulevya kuwa hadi sasa zimefikia 36 lakini hakuna taarifa zake.
Mwakyembe aliyasema hayo wakati akizungumza kwenye Kipindi cha Jenerali On Monday kilichorushwa na Kituo cha Televisheni cha Channel Ten juzi usiku.
Mwananchi iliwasiliana na Mkurugenzi wa Mashtaka, Elieza Feleshi kuhusiana na hilo, lakini hata hivyo simu yake ilikuwa haipatikani. Hata ilipofika ofisini kwake, ilielezwa kuwa alikuwa kwenye mkutano.
Kamanda wa Kikosi cha Kuzuia Dawa za Kulevya, Godfrey Nzowa alipotafutwa jana kuzungumzia hali hiyo, simu yake ilikuwa haipatikani.
“Kila anayekamatwa lazima achukuliwe hatua stahiki kwa kosa lake na hakuna sababu ya kuleana wala kuogopana,” alisema Dk Mwakyembe ambaye ametangaza kujitoa muhanga kupambana na mtandao wa dawa za kulevya nchini.
Mwakyembe aliyekuwa akizungumzia mapambano hayo aliyoyaanzisha ya dawa za kulevya, alirejea sakata la kuvushwa dawa za kulevya Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere, JNIA alisema: “Wote tumewafukuza kazi kwa sababu walihusika kupitisha dawa hizo.”
Hata hivyo, Mkurungenzi wa JNIA, Moses Malaki akizungumza na gazeti hili, alisema juzi kuwa utaratibu wa kuwapatia barua zao umekamilika na sasa kinachofuata ni utaratibu wa kuunda tume ambao utafanyika wakati wowote kwa ajili ya uchunguzi na kuwahoji.
Wafanyakazi hao wa JNIA, wanatuhumiwa kula njama za kupitisha kilo 150 za dawa za kulevya aina ya Crystal Methamphetamine.
Dk Mwakyembe alisema pia kuwa watu hao watafukuzwa kazi pamoja na wahusika wengine. “Ule mkanda unaonyesha watu walivyokuwa wakihangaika siku ile pale. Kuna askari anaonekana anasaidia kupitisha mizigo kwenye mashine, huyu askari ni kazi yake hii?
“Wapo watu walikuwa wakihangaika huku na huko, yaani walikuwa hawatulii, ni kama sinema, wengine wako ‘bize’ na simu badala ya kufanya ukaguzi, sasa tumewafukuza...Najua wapo wengine, nasema kama mtu aliona, alisikia na hakusema naye atakwenda na maji.
Alisema amewasiliana na Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Emmanuel Nchimbi kwa ajili ya kufanikisha kazi hiyo. “Nimemwomba Waziri wa Mambo ya Ndani tufanye kazi na lazima tuumalize huu mtandao.”
Akizungumzia ukaguzi wa mizigo, Dk Mwakyembe alisema lazima mizigo yote ikaguliwe hata bandarini. “Pale Uwanja wa Ndege kuna mitambo pengine bora zaidi kuliko mahala pengine popote Afrika na kama haitoshi, tuongeze mingine zaidi.

Alipoulizwa kama atakuwa na ubavu wa kuzuia ‘unga’ wa vigogo, Mwakyembe alisema: “Kigogo yeyote atakayejitokeza nitamkamata tu...Ajitokeze sasa hivi aone. Nimeshangazwa na kilo 180 kupita, huu mtandao wa kipuuzi lazima kuuvunja.
“Asije mtu akatarajia kuchekewa, ataondoka. Atakayeruhusu mtu kupita na dawa za kulevya, tukibaini, ataondoka tu. Wako wengi wanatafuta kazi. Tulijiachia vya kutosha, na sasa basi.”
Akizungumzia hali ilivyo Bandarini kwa sasa, alisema wameimarisha udhibiti wa upotevu wa makontena. “Hali kwa sasa ni nzuri, ilikuwa aibu, kila siku makontena yanapotea, tulianzisha utaratibu, kontena likipotea kitengo kizima wanakatwa mishahara kulipia,” alisema.
Alisema pia kumeanzishwa utaratibu wa kukagua mizigo yote inayoingia na kutoka.

Friday, August 9, 2013

THAMANI : Ibrahimovic, Ronaldo watikisa Ulaya

Ibrahimovic                                                      
USAJILI wa wanasoka barani Ulaya umeanza kupamba moto, tumeanza kuona nyota kadhaa wakinaswa.
Wiki hii tumemshuhudia Neymar akinaswa kutoka Santos kwenda Barcelona kwa ada ya Euro 57 milioni, naye Jesuz Navas alihama kutoka Sevilla kwenda Manchester City kwa Pauni 17 milioni.
Huo ni mwanzo tu, huenda tukashuhudia usajili wa fedha nyingi zaidi, lakini je ni nani anayeongoza kwa kusajiliwa kwa fedha nyingi katika historia ya soka? Jibu ni Zlatan Ibrahimovic.
Mchezaji huyo kutoka Sweden ndiye kinara wa fedha nyingi na amehama kwenye klabu saba tangu mwaka 2002 na kufanya jumla ya usajili wake kuwa wa Euro 169.1 milioni.
Ibrahimovic alijiunga na PSG akitokea AC Milan katika dirisha la usajili la msimu uliiopita kwa Euro 23 milioni na hapo ndipo alitimiza klabu saba tangu alipoanza kuhama.
Mchezaji huyo alianza kwa kuondoka Malmo FF kwenda Ajax kwa ada ya Euro 9 milioni mwaka 2002, Juventus ililipa Euro 16 kwa klabu ya Ajax ili kumnasa mwaka 2004, nayo Inter Milan ilimnunua nyota huyo kutoka Juventus kwa Euro 24.8 milion (2006).
Baadaye Barcelona ilimnunua kwa Euro 69.5 milioni kutoka Inter Milan (2009). Usajili huo ulishika namba tatu katika historia ya fedha za usajili duniani. 
Mwaka 2011 aliondoka Barcelona kwenda AC Milan kwa Euro 27 milioni. Lakini Cristiano Ronaldo, aliyehama mara mbili tu kwenye maisha yake ya soka, anashika nafasi ya tano na amesajiliwa kwa jumla ya Euro 111.5 milioni.
Mchezaji huyo alitoka Sporting Lisbon kwenda Man United kisha akaondoka Old Trafford kwenda Real Madrid kwa Euro 94 milioni ukiwa ni usajili mkubwa zaidi kwa mara moja kuwahi kutokea duniani.
Nyota wa Ireland, Robbie Keane, ndiye mchezaji ambaye amehama klabu nyingi zaidi tangu mwaka 1999 ambapo ameibuka kwenye klabu tisa.

BENITEZ (CHUCHO) : Afariki akiacha penzi la sinema la mrembo wake

 Liseth akiwa ameshikilia picha ya mumewe, Benitez katika Uwanja wa Ndege wa Doha



STAA wa Ecuador na klabu ya Jaish ya Qatar, Christian Benitez,  aliyefariki wiki iliyopita, ameondoka duniani akiacha penzi tamu la mrembo, Liseth Chala, ambaye alimuoa katika ndoa ya utata mithili ya filamu ya kusisimua.
Penzi lao lilikuwa maarufu nchini Ecuador, si tu kutokana na umaarufu wao, bali kwa jinsi lilivyokuwa la dhati na ambalo limesababisha simanzi kubwa baada ya kufariki kwa Benitez akiwa Qatar.
Walikutana akiwa na miaka 12
Benitez alimuoa Liseth mwaka 2007. Mrembo huyo ni mmoja kati ya watoto watatu wa staa wa zamani wa Ecuador, Cleber Chala, 42, ambaye alistaafu soka mwaka 2008.
Wakati wakikutana, Liseth ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 23, alikuwa na miaka 12 tu. Wakati huo Benitez alikuwa na umri wa miaka 17 akichezea klabu ya Nacional ambayo pia baba yake Liseth, Kleber alikuwa akichezea.
Kutokana na hali hiyo, Cleber alikataa mwanaye asiwe na uhusiano na Benitez kutokana na umri wao kuwa mdogo na akampiga marufuku asimuone na binti yake popote pale iwe nyumbani au uwanjani.
Hata hivyo, Benitez ambaye baba yake mzazi, Ermen pia alikuwa mwanasoka maarufu nchini Ecuador aliendelea kubisha na katika hali ya kushangaza Benitez na Liseth walipanga mipango ya ndoa ya siri ingawa wazazi wao walianza kuwashitukia moja kwa moja.
Baada ya maongezi ya muda mrefu kati ya Benitez na Cleber, mwishowe Cleber aliondoa ugumu na kumruhusu Benitez kumuoa binti yake katika harusi ya bomani iliyofanyika nchini Ecuador Julai 2006. Wakati huo Liseth alikuwa na umri wa miaka 15 tu.
Hata hivyo, Benitez na Lisa walipewa sharti moja la kila mmoja kuendelea kuishi na wazazi wake. Wakati huo, baba yake Liseth alikuwa na umri wa miaka 35 tu, huku Benitez akiwa na umri wa miaka 20.
Kwa kuwa wote wawili walikuwa wanasoka mahiri, ghafla wakajikuta wakiwa marafiki. Mama yake Liseth alijikuta mwenye furaha baada ya kuongezeka kwa Benitez katika familia yao.
Liseth hakukacha shule baada ya kuolewa akiwa na umri wa miaka 15 tu. Aliendelea na maisha yake huku akisoma katika shule ya Colegio Lesval.

Hata hivyo aliweka wazi kwamba angeacha kuishi nyumbani na kwenda nje ya nchi kama Benitez angepata timu nje ya Ecuador.
Ndicho kilichofuata. Julai 2006 wakati Benitez aliposajiliwa na klabu ya Santos Laguna ya Ligi Kuu Mexico, Liseth alitimka nyumbani kwenda naye Mexico.
Hata hivyo, kabla ya kuondoka, walifunga rasmi ndoa ya kanisani katika eneo la Iglesia Guapulo mji mkuu wa Quito, Ecuador, wakati huo Liseth alikuwa na miaka 17.
Aliingia kanisani akitembea kwa madaha huku akiwa ameuegemea mkono wa baba yake mzazi.
Ampiga mkwara mumewe, nchi yafurahi
Liseth alipata watoto watatu na Benitez. Wawili kati ya hao ni pacha Roger Cristiano na Emily Guadalupe ambao aliwazaa akiwa na umri wa miaka 18, ilikuwa Agosti 10, 2009 katika Hospitali ya De la Mujer mjini Torreon, Mexico.
Katika pambano moja muhimu la timu ya taifa lake la Ecuador dhidi ya Colombia, Liseth akiwa na mimba ya miezi mitatu alisikika akimwambia mumewe: “Kama haufungi bao, usirudi hapa nyumbani.”
Siku iliyofuata magazeti yote nchini Ecuador yaliandika kichwa hicho cha habari. Benitez na wenzake walicheza soka maridadi na kuichapa Colombia huku Benitez mwenyewe akifunga bao moja na hivyo kuruhusiwa kurudi nyumbani baada ya mechi. Liseth alijifungua mtoto wa kike Desemba 12, 2012.
Benitez amfia Liseth mikononi
Baada ya kukipiga katika klabu ya Laguna, Benitez alienda kwa mkopo katika klabu ya Birmingham katika msimu wa 2009/ 2010, lakini mwisho wa msimu timu hizo mbili zikashindwa kuafikiana uhamisho wa kudumu na kumfanya Benitez arudi tena Mexico na Liseth.
Mwaka 2011, Benitez alirudi Ecuador na kuiwezesha klabu ya America kutwaa ubingwa wa Ecuador. Hata hivyo, msimu huu alipata dili ya kukipiga katika klabu ya Jaish nchini Qatar na huko ndipo mauti yalipomkuta.
Wiki iliyopita, Julai 28, Benitez aliichezea Jaish mechi ya kwanza akiingia dakika 10 za mwisho dhidi ya Qatar FC. Siku iliyofuata, Benitez alitoka ‘out’ akiwa na Liseth pamoja na watoto kwenda kula katika hoteli moja ya Qatar.

 Ghafla akaanza kusikia maumivu makali ya tumbo na kulalamika. Liseth alimpeleka hospitali moja ya Doha na saa chache baadaye akaanza kukosa hewa na kupumua kwa shida. Baada ya muda alitangazwa kuwa amekufa kutokana na matatizo ya moyo.
Kuna lawama kwamba Benitez hakuwa amepata matibabu timilifu mara baada ya kuwasili. Liseth alimpigia simu baba yake kumfahamisha kuhusu kifo hicho alfajiri ya Julai 29.
Kuzikwa Alhamisi Ecuador
Mwili wake ulisafirishwa juzi Jumapili kwenda mji mkuu wa Ecuador, Quito huku Liseth akiwa bega kwa bega na serikali ya Qatar ambayo kwa kushirikiana na klabu ya Jaish walikodi ndege ya kwenda Ecuador.
Mwili wa Benitez unatarajiwa kuagwa kwa heshima katika ukumbi unaochukua watu 16,000.
Mazishi yake yanatazamiwa kufanyika katika makaburi ya Monte Olivo ambayo yapo karibu na makazi ya timu ya taifa ya Ecuador.
Maelfu ya mashabiki, viongozi wa serikali, wachezaji wenzake, wanafamilia wanatazamiwa kuhudhuria mazishi hayo.
Liseth ambaye ni mpenzi wake wa moyoni tangu akiwa na umri wa miaka 12, anatazamiwa kuwaongoza watoto wake watatu kuweka udongo katika kaburi la mumewe ambaye ametoka naye mbali kimaisha.
Valencia ahudhuria, jezi yake yastaafishwa
Winga mahiri wa Manchester United, Antonio Valencia,  alikuwapo wakati wa kupokea mwili wa Benitez baada ya kuomba ruhusa kutoka kwa kocha wake, David Moyes.
Wawili hao walikuwa wachezaji tegemeo zaidi kwa Ecuador. Shirikisho la Soka la Ecuador pia limeamua kuistaafisha jezi namba 11 ya timu ya taifa hilo iliyokuwa inatumiwa na Benitez.

Jambazi sugu la ATM lanaswa Dar es Salaam

Raia wa Bulgaria akiwa chini ya Ulinzi baada ya kupata kichapo kwa kudaiwa kuiba fedha kwenye mashine ya kutolea fedha (ATM) ya BOA tawi la Mbezi Beach, jijini Dar es Salaam jana.           


     Msako wa wezi wa kwenye Mashine za Kutolea Fedha (ATM), umeanza kuzaa matunda baada ya raia wa Bulgaria kukamatwa akiiba kwenye ATM ya Bank of Africa (BOA), Tawi la Afrikana, Kinondoni, Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa taarifa za benki, mtuhumiwa huyo ambaye hakutajwa jina lake alikamatwa baada ya kamera maalumu zilizowekwa kwenye ATM za BOA, kumtambua kuwa ni mwizi sugu wa benki hiyo anayetafutwa.
Mmoja wa wafanyakazi wa benki hiyo ambaye hakupenda kutajwa jina kwa kuwa si msemaji, alisema tukio hilo lilitokea jana saa 12 asubuhi baada ya mtuhumiwa huyo kuwekewa mitambo maalumu ya kumnasa.
Alisema benki hiyo ilipelekewa malalamiko na baadhi ya wateja kwamba wakienda kutoa fedha kwenye ATM wanakuta akaunti zao hazina salio wakati wanaamini zilikuwa na fedha.
Chanzo hicho cha habari kilidai kuwa baada ya kupelekewa malalamiko hayo, waliweka mitambo maalumu ya kuwawezesha walinzi wa maeneo ya ATM za BOA kumbaini mtu atakayetoa fedha kwa njia ya wizi.
“Kama Benki tuliweka mtambo maalumu na mtuhumiwa huyo alionekana kwenye mtambo wetu, hivyo tuliwaagiza walinzi wetu watakapomwona mtu huyo wamkamate haraka sana,”alisema.
Alisema mtuhumiwa huyo alianza mchezo huo kwa muda mrefu ambapo kwa kutumia kadi za ATM zisizojulikana idadi yake, alikuwa anakwenda kwenye ATM mbalimbali za benki hiyo na kutoa fedha hadi Sh10 milioni.
Kuhusu tukio la jana, mmoja wa walinzi wa BOA aliyejitambulisha kwa jina moja la Frenky alisema mtuhumiwa huyo alipofika kwenye ATM hiyo aliingia na kuchukua fedha ambazo alizipeleka kwenye gari lake. Frenky alisema baada ya kupeleka fedha hizo, alirudi kwa mara ya pili ili achukue fedha nyingine ndipo walinzi hao walimkamata na kumfunga pingu.
“Huyu mtuhumiwa mwenye asili ya Kiarabu alifika na gari lake saa 12 asubuhi, aliingia kwenye ATM na kutoa fedha ambazo hazikujulikana ni shilingi ngapi na kuzipeleka kwenye gari lake, baadaye alirejea tena kwa ajili ya kutoa fedha zingine, wakati anaingia ndipo alipokamatwa na mlinzi aliyekuwa analinda hapo,” alisema Frenky.
Kamanda wa Polisi Kinondoni, Camilius Wambura alikiri kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa mtuhumiwa anashikiliwa na jeshi hilo huku uchunguzi dhidi yake ukiendelea.
“Ni kweli taarifa nimezipata, mtuhumiwa amekamatwa, bado hatujajua ni kiasi gani ambacho ameiba kwa kutumia mtandao, tunaendelea na uchunguzi,” alisema Wambura.
Tukio kama hili lilishawahi kutokea mkoani Mwanza Februari 19 mwaka huu na Jeshi la Polisi mkoani Mwanza kwa kushirikiana na maofisa ya Benki ya NMB liliwatia mbaroni watu watatu ambao walidaiwa kuiba kiasi cha Sh700 milioni kwa nyakati tofauti. 
    Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi, Christopher Fuime alisema watuhumiwa hao walinaswa baada ya kuwekewa mtego na maofisa wa benki na polisi saa 6 usiku wa Februari 19, mwaka huu na mtuhumiwa mmoja alibambwa akichukua fedha kwenye ATM ya NMB kwenye Tawi la PPF Plaza Mwanza.
Vifaa walivyokutwa navyo ni kadi bandia 194 za kuchukulia fedha katika ATM za NMB na kati yake kadi 95 zilikuwa na namba 0225152975 zilizotumia namba ya akaunti ya 2258103695 zenye jina na picha ya mtu anayedaiwa kuwa ni Moley L.P.
Kadi nyingine 99 zilikuwa na namba 0506056317 za akaunti namba 5068000322 zikitumia jina moja la Mnuo Z.E na picha moja.
Mbali na kadi hizo waliweza kunasa kadi 36 za Benki ya DTB ambazo kati yake kadi 18 zilikuwa na jina moja la Kelvini G Gratias na namba 20497883, kadi 12 zilitumika jina la J.Paul zenye akaunti namba 2049783 huku kadi sita zikitumia jina moja la Joseph Donald akaunti namba 2049783.
Kadi nyingine tatu zenye maandishi ya Download list na nyingine ikiwa ni kadi ya Visa ya Benki ya KCB yenye namba 413546040003827 zilitumia jina la Elikana Zacharia.

Thursday, August 1, 2013

Serikali yatangaza wanaokwenda ualimu

                                                                                                                                   

        
Dar es Salaam. Serikali imetangaza majina ya wanafunzi 18,754 waliochaguliwa kujiunga na vyuo vya ualimu vilivyo chini yake ikiwa ni ongezeko la wanafunzi 1,659 ikilinganishwa na 17,095 waliochaguliwa mwaka jana.
Kati ya wanafunzi hao, 11,806 wamechaguliwa kusomea ngazi ya cheti (Grade A) na 6,948 watasoma katika ngazi ya stashahada.
Wanafunzi 363 wamechaguliwa kusoma elimu maalumu kwa ngazi ya cheti huku 57 wakisoma elimu hiyo kwa ngazi ya stashahada.
Akizungumza na mwandishi wetu jana, Msemaji wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Ntambi Bunyazu alisema wanafunzi wanatakiwa kuripoti kwenye vyuo walivyopangiwa kuanzia Agosti 15, mwaka huu.
“Usajili utafungwa Agosti 25 saa 12:00 jioni, ‘Joining instructions’ (fomu ya maelekezo ya kujiunga) zitatumwa kwa wahusika kupitia anuani zao.... fomu hizi pia zinapatikana kwenye tovuti ya Wizara ya Elimu na mafunzo ya Ufundi,” alisema.
Taarifa ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi iliyotolewa baadaye jana ilisema kuwa wanafunzi waliochaguliwa wanatakiwa kufika vyuoni wakiwa na vyeti halisi vya kidato cha nne na cha sita vinavyotolewa na Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta) , ada ya muhula wa kwanza Sh100,000 au Sh200,000 kwa mwaka.
Wanatakiwa kuwa na “Sare ya chuo kulingana na maelekezo ya chuo husika, fedha za tahadhari chuoni na matumizi binafsi,” inasema taarifa hiyo.
Taarifa hiyo inaeleza pia kuwa wakuu wa vyuo wanatakiwa kuhakikisha wanafunzi wanaosajiliwa ni wale waliopo kwenye orodha iliyotolewa na wizara na si vinginevyo.
Wengi wa wanafunzi hawa ni wale waliohitimu kidato cha nne mwaka 2012 na kidato cha sita mwaka huu. Kwa upande wa wale wa kidato cha nne, matokeo yaliyotangazwa na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi yalionyesha kuwa watahiniwa 159,609 wa shule walifaulu kwa daraja la kwanza mpaka la nne.
Inaonyesha pia kuwa kwa upande wa Tanzania Bara, wanafunzi 34,599 walifaulu kwa daraja la kwanza mpaka la tatu na kati yake waliochaguliwa kujiunga na kidato cha tano na vyuo vya ufundi walikuwa ni 34,213.
Kwa upande wa matokeo ya kidato cha sita mwaka huu, watahiniwa waliofaulu mtihani huo walikuwa ni 44,366 kati yao 40,242 wakiwa ni wa shule. Matokeo hayo yanaonyesha pia kuwa, watahiniwa 35,880 ndiyo waliofaulu kwa daraja la kwanza mpaka la tatu.
Kwa mujibu wa Kitabu cha Takwimu cha Wizara ya Elimu (Best), mwaka 2012 wanafunzi 17,095 walichaguliwa kujiunga na vyuo mbalimbali vya ualimu nchini.
Kutokana na takwimu hizo, kuna uwezekano mkubwa kwamba wanaokwenda kusoma ngazi ya cheti wanatoka kwenye kundi la wanafunzi waliopata daraja la nne.
Wanafunzi waliopata daraja la nne kwenye mtihani wa kidato cha nne mwaka jana ni 124,260.
Baada ya kutangaza majina ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha tano pamoja na vyuo vya ufundi, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo aliliambia gazeti hili kuwa wanafunzi waliopata daraja la nne katika kiwango cha alama 27 watachaguliwa kujiunga na vyuo vya ualimu endapo wataomba.
“Vigezo vya kujiunga na kidato cha tano na vile vya vyuo vya ualimu ni tofauti. Kidato cha tano mwisho anatakiwa mtu mwenye alama 25 na masomo yake matatu yawe sawa, ualimu ni alama 27.
“Mwanzoni walikuwa wanakwenda wenye alama 28, lakini mwaka jana tukasema hapana, iwe alama 27 na tutachukua kuanzia waliomaliza shule mwaka 2008 kama wataomba, kwa sasa hivi watu wanaendelea na kazi ya kuwachagua,” alisema Mulugo.
Kwa muda mrefu, wadau wa elimu wamekuwa wakipiga kelele kuhusu wanafunzi wanaochaguliwa kusomea ualimu nchini wakitaka nafasi hiyo ichukuliwe na wale wanaofanya vizuri kwenye masomo yao.