Instagram

Friday, August 9, 2013

BENITEZ (CHUCHO) : Afariki akiacha penzi la sinema la mrembo wake

 Liseth akiwa ameshikilia picha ya mumewe, Benitez katika Uwanja wa Ndege wa Doha



STAA wa Ecuador na klabu ya Jaish ya Qatar, Christian Benitez,  aliyefariki wiki iliyopita, ameondoka duniani akiacha penzi tamu la mrembo, Liseth Chala, ambaye alimuoa katika ndoa ya utata mithili ya filamu ya kusisimua.
Penzi lao lilikuwa maarufu nchini Ecuador, si tu kutokana na umaarufu wao, bali kwa jinsi lilivyokuwa la dhati na ambalo limesababisha simanzi kubwa baada ya kufariki kwa Benitez akiwa Qatar.
Walikutana akiwa na miaka 12
Benitez alimuoa Liseth mwaka 2007. Mrembo huyo ni mmoja kati ya watoto watatu wa staa wa zamani wa Ecuador, Cleber Chala, 42, ambaye alistaafu soka mwaka 2008.
Wakati wakikutana, Liseth ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 23, alikuwa na miaka 12 tu. Wakati huo Benitez alikuwa na umri wa miaka 17 akichezea klabu ya Nacional ambayo pia baba yake Liseth, Kleber alikuwa akichezea.
Kutokana na hali hiyo, Cleber alikataa mwanaye asiwe na uhusiano na Benitez kutokana na umri wao kuwa mdogo na akampiga marufuku asimuone na binti yake popote pale iwe nyumbani au uwanjani.
Hata hivyo, Benitez ambaye baba yake mzazi, Ermen pia alikuwa mwanasoka maarufu nchini Ecuador aliendelea kubisha na katika hali ya kushangaza Benitez na Liseth walipanga mipango ya ndoa ya siri ingawa wazazi wao walianza kuwashitukia moja kwa moja.
Baada ya maongezi ya muda mrefu kati ya Benitez na Cleber, mwishowe Cleber aliondoa ugumu na kumruhusu Benitez kumuoa binti yake katika harusi ya bomani iliyofanyika nchini Ecuador Julai 2006. Wakati huo Liseth alikuwa na umri wa miaka 15 tu.
Hata hivyo, Benitez na Lisa walipewa sharti moja la kila mmoja kuendelea kuishi na wazazi wake. Wakati huo, baba yake Liseth alikuwa na umri wa miaka 35 tu, huku Benitez akiwa na umri wa miaka 20.
Kwa kuwa wote wawili walikuwa wanasoka mahiri, ghafla wakajikuta wakiwa marafiki. Mama yake Liseth alijikuta mwenye furaha baada ya kuongezeka kwa Benitez katika familia yao.
Liseth hakukacha shule baada ya kuolewa akiwa na umri wa miaka 15 tu. Aliendelea na maisha yake huku akisoma katika shule ya Colegio Lesval.

Hata hivyo aliweka wazi kwamba angeacha kuishi nyumbani na kwenda nje ya nchi kama Benitez angepata timu nje ya Ecuador.
Ndicho kilichofuata. Julai 2006 wakati Benitez aliposajiliwa na klabu ya Santos Laguna ya Ligi Kuu Mexico, Liseth alitimka nyumbani kwenda naye Mexico.
Hata hivyo, kabla ya kuondoka, walifunga rasmi ndoa ya kanisani katika eneo la Iglesia Guapulo mji mkuu wa Quito, Ecuador, wakati huo Liseth alikuwa na miaka 17.
Aliingia kanisani akitembea kwa madaha huku akiwa ameuegemea mkono wa baba yake mzazi.
Ampiga mkwara mumewe, nchi yafurahi
Liseth alipata watoto watatu na Benitez. Wawili kati ya hao ni pacha Roger Cristiano na Emily Guadalupe ambao aliwazaa akiwa na umri wa miaka 18, ilikuwa Agosti 10, 2009 katika Hospitali ya De la Mujer mjini Torreon, Mexico.
Katika pambano moja muhimu la timu ya taifa lake la Ecuador dhidi ya Colombia, Liseth akiwa na mimba ya miezi mitatu alisikika akimwambia mumewe: “Kama haufungi bao, usirudi hapa nyumbani.”
Siku iliyofuata magazeti yote nchini Ecuador yaliandika kichwa hicho cha habari. Benitez na wenzake walicheza soka maridadi na kuichapa Colombia huku Benitez mwenyewe akifunga bao moja na hivyo kuruhusiwa kurudi nyumbani baada ya mechi. Liseth alijifungua mtoto wa kike Desemba 12, 2012.
Benitez amfia Liseth mikononi
Baada ya kukipiga katika klabu ya Laguna, Benitez alienda kwa mkopo katika klabu ya Birmingham katika msimu wa 2009/ 2010, lakini mwisho wa msimu timu hizo mbili zikashindwa kuafikiana uhamisho wa kudumu na kumfanya Benitez arudi tena Mexico na Liseth.
Mwaka 2011, Benitez alirudi Ecuador na kuiwezesha klabu ya America kutwaa ubingwa wa Ecuador. Hata hivyo, msimu huu alipata dili ya kukipiga katika klabu ya Jaish nchini Qatar na huko ndipo mauti yalipomkuta.
Wiki iliyopita, Julai 28, Benitez aliichezea Jaish mechi ya kwanza akiingia dakika 10 za mwisho dhidi ya Qatar FC. Siku iliyofuata, Benitez alitoka ‘out’ akiwa na Liseth pamoja na watoto kwenda kula katika hoteli moja ya Qatar.

 Ghafla akaanza kusikia maumivu makali ya tumbo na kulalamika. Liseth alimpeleka hospitali moja ya Doha na saa chache baadaye akaanza kukosa hewa na kupumua kwa shida. Baada ya muda alitangazwa kuwa amekufa kutokana na matatizo ya moyo.
Kuna lawama kwamba Benitez hakuwa amepata matibabu timilifu mara baada ya kuwasili. Liseth alimpigia simu baba yake kumfahamisha kuhusu kifo hicho alfajiri ya Julai 29.
Kuzikwa Alhamisi Ecuador
Mwili wake ulisafirishwa juzi Jumapili kwenda mji mkuu wa Ecuador, Quito huku Liseth akiwa bega kwa bega na serikali ya Qatar ambayo kwa kushirikiana na klabu ya Jaish walikodi ndege ya kwenda Ecuador.
Mwili wa Benitez unatarajiwa kuagwa kwa heshima katika ukumbi unaochukua watu 16,000.
Mazishi yake yanatazamiwa kufanyika katika makaburi ya Monte Olivo ambayo yapo karibu na makazi ya timu ya taifa ya Ecuador.
Maelfu ya mashabiki, viongozi wa serikali, wachezaji wenzake, wanafamilia wanatazamiwa kuhudhuria mazishi hayo.
Liseth ambaye ni mpenzi wake wa moyoni tangu akiwa na umri wa miaka 12, anatazamiwa kuwaongoza watoto wake watatu kuweka udongo katika kaburi la mumewe ambaye ametoka naye mbali kimaisha.
Valencia ahudhuria, jezi yake yastaafishwa
Winga mahiri wa Manchester United, Antonio Valencia,  alikuwapo wakati wa kupokea mwili wa Benitez baada ya kuomba ruhusa kutoka kwa kocha wake, David Moyes.
Wawili hao walikuwa wachezaji tegemeo zaidi kwa Ecuador. Shirikisho la Soka la Ecuador pia limeamua kuistaafisha jezi namba 11 ya timu ya taifa hilo iliyokuwa inatumiwa na Benitez.

0 comments: