Liseth akiwa ameshikilia picha ya mumewe, Benitez katika Uwanja wa Ndege wa Doha
STAA wa Ecuador na klabu ya Jaish ya Qatar, Christian Benitez,
aliyefariki wiki iliyopita, ameondoka duniani akiacha penzi tamu la
mrembo, Liseth Chala, ambaye alimuoa katika ndoa ya utata mithili ya
filamu ya kusisimua.
Penzi lao lilikuwa maarufu nchini Ecuador, si tu
kutokana na umaarufu wao, bali kwa jinsi lilivyokuwa la dhati na ambalo
limesababisha simanzi kubwa baada ya kufariki kwa Benitez akiwa Qatar.
Walikutana akiwa na miaka 12
Benitez alimuoa Liseth mwaka 2007. Mrembo huyo ni
mmoja kati ya watoto watatu wa staa wa zamani wa Ecuador, Cleber Chala,
42, ambaye alistaafu soka mwaka 2008.
Wakati wakikutana, Liseth ambaye kwa sasa ana umri
wa miaka 23, alikuwa na miaka 12 tu. Wakati huo Benitez alikuwa na umri
wa miaka 17 akichezea klabu ya Nacional ambayo pia baba yake Liseth,
Kleber alikuwa akichezea.
Kutokana na hali hiyo, Cleber alikataa mwanaye
asiwe na uhusiano na Benitez kutokana na umri wao kuwa mdogo na akampiga
marufuku asimuone na binti yake popote pale iwe nyumbani au uwanjani.
Hata hivyo, Benitez ambaye baba yake mzazi, Ermen
pia alikuwa mwanasoka maarufu nchini Ecuador aliendelea kubisha na
katika hali ya kushangaza Benitez na Liseth walipanga mipango ya ndoa ya
siri ingawa wazazi wao walianza kuwashitukia moja kwa moja.
Baada ya maongezi ya muda mrefu kati ya Benitez na
Cleber, mwishowe Cleber aliondoa ugumu na kumruhusu Benitez kumuoa
binti yake katika harusi ya bomani iliyofanyika nchini Ecuador Julai
2006. Wakati huo Liseth alikuwa na umri wa miaka 15 tu.
Hata hivyo, Benitez na Lisa walipewa sharti moja
la kila mmoja kuendelea kuishi na wazazi wake. Wakati huo, baba yake
Liseth alikuwa na umri wa miaka 35 tu, huku Benitez akiwa na umri wa
miaka 20.
Kwa kuwa wote wawili walikuwa wanasoka mahiri,
ghafla wakajikuta wakiwa marafiki. Mama yake Liseth alijikuta mwenye
furaha baada ya kuongezeka kwa Benitez katika familia yao.
Liseth hakukacha shule baada ya kuolewa akiwa na
umri wa miaka 15 tu. Aliendelea na maisha yake huku akisoma katika shule
ya Colegio Lesval.
Hata hivyo aliweka wazi kwamba angeacha kuishi nyumbani na kwenda nje ya nchi kama Benitez angepata timu nje ya Ecuador.
Ndicho kilichofuata. Julai 2006 wakati Benitez
aliposajiliwa na klabu ya Santos Laguna ya Ligi Kuu Mexico, Liseth
alitimka nyumbani kwenda naye Mexico.
Hata hivyo, kabla ya kuondoka, walifunga rasmi
ndoa ya kanisani katika eneo la Iglesia Guapulo mji mkuu wa Quito,
Ecuador, wakati huo Liseth alikuwa na miaka 17.
Aliingia kanisani akitembea kwa madaha huku akiwa ameuegemea mkono wa baba yake mzazi.
Ampiga mkwara mumewe, nchi yafurahi
Liseth alipata watoto watatu na Benitez. Wawili
kati ya hao ni pacha Roger Cristiano na Emily Guadalupe ambao aliwazaa
akiwa na umri wa miaka 18, ilikuwa Agosti 10, 2009 katika Hospitali ya
De la Mujer mjini Torreon, Mexico.
Katika pambano moja muhimu la timu ya taifa lake
la Ecuador dhidi ya Colombia, Liseth akiwa na mimba ya miezi mitatu
alisikika akimwambia mumewe: “Kama haufungi bao, usirudi hapa nyumbani.”
Siku iliyofuata magazeti yote nchini Ecuador
yaliandika kichwa hicho cha habari. Benitez na wenzake walicheza soka
maridadi na kuichapa Colombia huku Benitez mwenyewe akifunga bao moja na
hivyo kuruhusiwa kurudi nyumbani baada ya mechi. Liseth alijifungua
mtoto wa kike Desemba 12, 2012.
Benitez amfia Liseth mikononi
Baada ya kukipiga katika klabu ya Laguna, Benitez
alienda kwa mkopo katika klabu ya Birmingham katika msimu wa 2009/ 2010,
lakini mwisho wa msimu timu hizo mbili zikashindwa kuafikiana uhamisho
wa kudumu na kumfanya Benitez arudi tena Mexico na Liseth.
Mwaka 2011, Benitez alirudi Ecuador na kuiwezesha
klabu ya America kutwaa ubingwa wa Ecuador. Hata hivyo, msimu huu
alipata dili ya kukipiga katika klabu ya Jaish nchini Qatar na huko
ndipo mauti yalipomkuta.
Wiki iliyopita, Julai 28, Benitez aliichezea Jaish
mechi ya kwanza akiingia dakika 10 za mwisho dhidi ya Qatar FC. Siku
iliyofuata, Benitez alitoka ‘out’ akiwa na Liseth pamoja na watoto
kwenda kula katika hoteli moja ya Qatar.
Ghafla akaanza kusikia maumivu makali ya tumbo na
kulalamika. Liseth alimpeleka hospitali moja ya Doha na saa chache
baadaye akaanza kukosa hewa na kupumua kwa shida. Baada ya muda
alitangazwa kuwa amekufa kutokana na matatizo ya moyo.
Kuna lawama kwamba Benitez hakuwa amepata matibabu
timilifu mara baada ya kuwasili. Liseth alimpigia simu baba yake
kumfahamisha kuhusu kifo hicho alfajiri ya Julai 29.
Kuzikwa Alhamisi Ecuador
Mwili wake ulisafirishwa juzi Jumapili kwenda mji
mkuu wa Ecuador, Quito huku Liseth akiwa bega kwa bega na serikali ya
Qatar ambayo kwa kushirikiana na klabu ya Jaish walikodi ndege ya kwenda
Ecuador.
Mwili wa Benitez unatarajiwa kuagwa kwa heshima katika ukumbi unaochukua watu 16,000.
Mazishi yake yanatazamiwa kufanyika katika makaburi ya Monte Olivo ambayo yapo karibu na makazi ya timu ya taifa ya Ecuador.
Maelfu ya mashabiki, viongozi wa serikali, wachezaji wenzake, wanafamilia wanatazamiwa kuhudhuria mazishi hayo.
Liseth ambaye ni mpenzi wake wa moyoni tangu akiwa
na umri wa miaka 12, anatazamiwa kuwaongoza watoto wake watatu kuweka
udongo katika kaburi la mumewe ambaye ametoka naye mbali kimaisha.
Valencia ahudhuria, jezi yake yastaafishwa
Winga mahiri wa Manchester United, Antonio
Valencia, alikuwapo wakati wa kupokea mwili wa Benitez baada ya kuomba
ruhusa kutoka kwa kocha wake, David Moyes.
Wawili hao walikuwa wachezaji tegemeo zaidi kwa
Ecuador. Shirikisho la Soka la Ecuador pia limeamua kuistaafisha jezi
namba 11 ya timu ya taifa hilo iliyokuwa inatumiwa na Benitez.